MTU
mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Dismas Macha, amekamatwa akiwa na
nyaraka mbalimbali za Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), baada
kubainika ni daktari ‘feki’ katika Kitengo cha Mifupa (MOI), jijini Dar
es Salaam.
Akizungumza
na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka
MOI, Frank Matua, alisema kuwa Macha ni daktari feki wa siku nyingi
ambaye aliwahi kufanya utapeli kama huo MNH.
Alisema
hadi daktari huyo anakamatwa, aliwekewa mtego baada ya kudanganya
kwamba ana dada yake aliyefariki nchini India akiwa kwenye matibabu,
hivyo alikuwa na orodha ya Maprofesa kadhaa iliyoonyesha kumchangia na
alikuwa akipita wodini ili kuchangisha fedha aweze kusafirisha mwili wa
marehemu huyo.
Matua,
alisema baada ya wafanyakazi wa MOI pamoja na wagonjwa kumbaini kuwa ni
mwongo, ndipo walimposubiri hadi alipofika na alipoingia tu ndani
walimfungia na kuanza kumhoji, ambako alikiri kufanya utapeli huo wa
udaktari feki na alikiri kuwatapeli wagonjwa mbalimbali, hivyo walipiga
polisi ambao walifika na kumchukua kwa mahojiano zaidi.
Alifafanua
kuwa, wakati Macha anafanya utapeli MNH aliwahi kukamatwa na
kuchukuliwa hatua za kisheria lakini baadaye alirudi tena na kuingia
katika chuo kikuu cha afya na sayansi shirikishi Muhimbili (MUHAS),
akijifanya kwamba yeye ni mwanafuzi lakini baada ya kugunduliwa
alihamia MOI.
Kutokana
ana tukio hilo, Matua alisema jukumu la MNH ni kuhakikisha usalama
unazingatiwa kutokana kwa kuimarisha ulinzi uliopo katika hospitali
hiyo, ingawa vitendo vingine kama hivyo na ujambazi si mara ya kwanza
kutokea hospitalini hapo.
Alitoa wito kwa Watanzania, kuwa makini na matapeli hasa katika hospitali mbalimbali hapa nchini.
MWISHO
