Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) mkoa wa Kilimanjaro, kimepitisha azimio la kwenda mahakamani
kusimamisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Desemba 14 mwaka
huu, hadi hapo Tamisemi itakapotoa haki ya kurejeshwa kwa wapiga kura
517 na wagombea wake 52 walioenguliwa.
Azimio
hilo la Chadema la kupinga uchaguzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Moshi, limetolewa wakati zikiwa zimebaki siku nne tu, uchaguzi huo
ufanyike nchini kote.
Katibu
wa Chama hicho mkoani hapa, Basil Lema, alisema tayari wamemwagiza
Mwanasheria wao kuandaa hoja za kisheria kisha kufungua kesi ya kupinga
uchaguzi huo leo kutafuta haki ya wananchi na wagombea wa nafasi
mbalimbali walioenguliwa, hivyo kuwakosesha kutimiza haki yao ya
kikatiba.
“Jumla
ya wagombea 52 wa nafasi mbalimbali wanaotokana na Chadema mkoa wa
Kilimanjaro, wameenguliwa kwa makusudi kutokana na kasoro zilizopo
kwenye fomu ya kuomba uongozi, lakini pia wamo wapiga kura 517
walioenguliwa na wasimamizi wa uchaguzi kwa madai ya kuwa si wakazi
halali na wengine wakitajwa kuwa si raia. Tunaamini wapo wanaoonewa,”
alisema Lema.
Katika
Kata ya Mawenzi mjini Moshi, wananchi 159 kati ya 162 waliojiandikisha
kupiga kura, wameenguliwa baada yakudaiwa kwamba siyo wakazi halali wa
eneo hilo. Aidha, kwenye kundi hilo la wanaodaiwa kuwa si wakazi, imo
familia ya watu wanne ya Diwani wa Chadema, Hawa Mushi.
Kwa
mujibu wa Lema, hali ni mbaya zaidi katika Jimbo la Same Magharibi, kwa
kuwa kwenye Kata tatu zenye jumla ya wagombea wake 21 walioomba uongozi
wameenguliwa wote na hivyo kutoa mwanya kwa Chama cha Mapinduzi (CCM)
kupita bila kupingwa.
“Kwenye
jimbo hilo hilo, wananchi 180 wa Kijiji cha Marwa, Kata ya Ruvu
wameenguliwa baada ya kujiandikisha kwa madai kwamba wao si wakazi wa
eneo hilo. Hizi ni rafu ambazo wenzetu CCM wanatuchezea Ukawa ili
kuuhadaa umma kwamba Muungano wetu hauna tija kisiasa,” alisisitiza
Katibu huyo.
VIA>Chademablog